Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Daudi. Nijibu nikuitapo, Ee Mungu wangu mwenye haki! Nipumzishe katika shida zangu; nirehemu, usikie ombi langu.
2
Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu kuwa aibu mpaka lini? Mtapenda udanganyifu na kufuata miungu ya uongo mpaka lini?
3
Fahamuni hakika kwamba Bwana amewatenga wale wamchao kwa ajili yake; Bwana atanisikia nimwitapo.
4
Katika hasira yako, usitende dhambi. Mkiwa vitandani mwenu, mtulie kimya mkiichunguza mioyo yenu.
5
Toeni dhabihu zilizo haki; mtegemeeni Bwana.
6
Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye kutuonyesha jema lolote?” Ee Bwana, tuangazie nuru ya uso wako.
7
Wewe umejaza moyo wangu kwa furaha kubwa kuliko watu waliopata nafaka na divai kwa wingi.
8
Nitajilaza chini na kulala kwa amani, kwa kuwa wewe peke yako, Ee Bwana, waniwezesha kukaa kwa salama.