Psa 8

? AI
1
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, Bwana wetu, tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Umeuweka utukufu wako juu ya mbingu.
2
Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao umeamuru sifa, kwa sababu ya watesi wako, kumnyamazisha adui na mlipiza kisasi.
3
Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota, ulizoziratibisha,
4
mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria, binadamu ni nani hata unamjali?
5
Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni, ukamvika taji ya utukufu na heshima.
6
Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako; umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.
7
Mifugo na makundi yote pia, naam, na wanyama wa kondeni,
8
ndege wa angani na samaki wa baharini, naam, kila kiogeleacho katika njia za bahari.
9
Ee Bwana, Bwana wetu, tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
Global Bible Tools - Collaborative Bible translation platform