Psa 65

? AI
1
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Wimbo. Ee Mungu, sifa zakungojea katika Sayuni; kwako wewe nadhiri zetu zitatimizwa.
2
Ewe usikiaye maombi, kwako wewe watu wote watakuja.
3
Tulipokuwa tumefunikwa kabisa na dhambi, wewe ulisamehe makosa yetu.
4
Heri wale uliowachagua na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako! Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako, mema ya Hekalu lako takatifu.
5
Unatujibu kwa matendo ya kushangaza ya haki, Ee Mungu Mwokozi wetu, tumaini la miisho yote ya duniani na la bahari zilizo mbali sana,
6
uliyeumba milima kwa uwezo wako, ukiwa umejivika nguvu,
7
uliyenyamazisha dhoruba za bahari, ngurumo za mawimbi yake, na ghasia za mataifa.
8
Wale wanaoishi mbali sana wanaogopa maajabu yako, kule asubuhi ipambazukiapo na kule jioni inakofifilia umeziita nyimbo za furaha.
9
Waitunza nchi na kuinyeshea, waitajirisha kwa wingi. Vijito vya Mungu vimejaa maji ili kuwapa watu nafaka, kwa maana wewe umeviamuru.
10
Umeilowesha mifereji yake na kusawazisha kingo zake; umeilainisha kwa manyunyu na kuibariki mimea yake.
11
Umeuvika mwaka taji ya baraka, magari yako yanafurika kwa wingi.
12
Mbuga za majani za jangwani umezineemesha; vilima vimevikwa furaha.
13
Penye nyanda za malisho pamejaa makundi ya wanyama, na mabonde yamepambwa kwa mavuno; vyote vinashangilia kwa furaha na kuimba.
Global Bible Tools - Collaborative Bible translation platform