Neno kuhusu Moabu: Ari iliyo Moabu imeangamizwa: imeharibiwa kwa usiku mmoja! Kiri iliyo Moabu imeangamizwa, imeharibiwa kwa usiku mmoja!
2
Diboni anakwea hadi kwenye hekalu lake, mpaka mahali pake pa juu ili walie, Moabu anaombolezea Nebo na Medeba. Kila kichwa kimenyolewa na kila ndevu limeondolewa.
3
Wamevaa nguo za magunia barabarani, juu ya mapaa na kwenye viwanja wote wanaomboleza, wamelala kifudifudi kwa kulia.
4
Heshboni na Eleale wanalia, sauti zao zinasikika hadi Yahazi. Kwa hiyo watu wenye silaha wa Moabu wanapiga kelele, nayo mioyo yao imezimia.
5
Moyo wangu unamlilia Moabu; wakimbizi wake wanakimbilia Soari, hadi Eglath-Shelishiya. Wanapanda njia ya kwenda Luhithi, wanakwenda huku wanalia; barabarani iendayo Horonaimu wanaombolezea maangamizi yao.
6
Maji ya Nimrimu yamekauka na majani yamenyauka; mimea imekauka wala hakuna kitu chochote kibichi kilichobaki.
7
Kwa hiyo mali waliyoipata na kujiwekea akiba wamezichukua na kuvuka Bonde la Mierebi.
8
Mwangwi wa kilio chao umefika hadi mpakani mwa Moabu, kilio chao cha huzuni kimefika hadi Eglaimu, maombolezo yao hadi Beer-Elimu.
9
Maji ya Dimoni yamejaa damu, lakini bado nitaleta pigo jingine juu ya Dimoni: simba juu ya wakimbizi wa Moabu na juu ya wale wanaobaki katika nchi.