Hili ndilo neno la Bwana lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaishambulia Gaza:
2
Hili ndilo asemalo Bwana: “Tazama jinsi maji yanavyoinuka huko kaskazini, yatakuwa mafuriko yenye nguvu sana. Yataifurikia nchi na vitu vyote vilivyomo ndani yake, miji na wale waishio ndani yake. Watu watapiga kelele; wote waishio katika nchi wataomboleza
3
kwa sauti ya kwato za farasi waendao mbio, kwa sauti ya magari ya adui na mngurumo wa magurudumu yake. Baba hawatageuka kuwasaidia watoto wao, mikono yao italegea.
4
Kwa maana siku imewadia kuwaangamiza Wafilisti wote na kuwakatilia mbali walionusurika wote ambao wangeweza kusaidia Tiro na Sidoni. Bwana anakaribia kuwaangamiza Wafilisti, mabaki toka pwani za Kaftori.
5
Gaza atanyoa kichwa chake katika kuomboleza, Ashkeloni atanyamazishwa. Enyi mabaki kwenye tambarare, mtajikatakata wenyewe mpaka lini?
6
“Mnalia, ‘Aa, upanga wa Bwana, utaendelea mpaka lini ndipo upumzike? Rudi ndani ya ala yako; acha na utulie.’
7
Lakini upanga utatuliaje wakati Bwana ameuamuru, wakati ameuagiza kuishambulia Ashkeloni pamoja na pwani yake?”