Akiwa ndani ya tumbo la nyangumi, Yona alimwomba Bwana Mungu wake.
2
Akasema: “Katika shida yangu nalimwita Bwana, naye akanijibu. Kutoka kina cha kaburi niliomba msaada, nawe ukasikiliza kilio changu.
3
Ulinitupa kwenye kilindi, ndani kabisa ya moyo wa bahari, mikondo ya maji ilinizunguka, mawimbi yako yote na viwimbi vilipita juu yangu.
4
Nikasema, ‘Nimefukuziwa mbali na uso wako, hata hivyo nitatazama tena kuelekea Hekalu lako takatifu.’
5
Maji yaliyonimeza yalinitisha, kilindi kilinizunguka; mwani ulijisokota kichwani pangu.
6
Nilizama chini sana mpaka pande za mwisho za milima, makomeo ya hiyo nchi yalinifungia hata milele. Lakini uliuleta uhai wangu kutoka shimoni, Ee Bwana Mungu wangu.
7
“Wakati uhai wangu ulipokuwa unatoka, nilikukumbuka wewe, Bwana, nayo maombi yangu yalikufikia wewe, katika Hekalu lako takatifu.
8
“Wale watu wanaongʼangʼana na sanamu zisizofaa hupoteza neema ile ambayo ingekuwa yao.
9
Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani, nitakutolea dhabihu. Lile nililowekea nadhiri nitalitimiza. Wokovu watoka kwa Bwana.”
10
Basi Bwana akamwamuru yule nyangumi, naye akamtapika Yona katika nchi kavu.