Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, usinikemee katika hasira yako, wala usiniadhibu katika ghadhabu yako.
2
Unirehemu Bwana, kwa maana nimedhoofika; Ee Bwana, uniponye, kwa maana mifupa yangu ina maumivu makali.
3
Nafsi yangu ina uchungu mwingi. Mpaka lini, Ee Bwana, mpaka lini?
4
Geuka Ee Bwana, unikomboe, uniokoe kwa sababu ya fadhili zako.
5
Hakuna mtu anayekukumbuka akiwa amekufa. Ni nani awezaye kukusifu akiwa kuzimu?
6
Nimechakaa kwa kulia kwa huzuni; usiku kucha nafurikisha kitanda changu kwa machozi; nimelowesha viti vyangu vya fahari kwa machozi.
7
Macho yangu yamedhoofika kwa kuhuzunika, yamedhoofika kwa sababu ya adui zangu wote.
8
Kaeni mbali nami, ninyi nyote mtendao mabaya, kwa maana Bwana amesikia kulia kwangu.
9
Bwana amesikia kilio changu kwa huruma, Bwana amekubali sala yangu.
10
Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, watarudi nyuma kwa aibu ya ghafula.