Psa 112

? AI
1
Msifuni Bwana. Heri mtu yule amchaye Bwana, mtu yule apendezwaye sana na amri zake.
2
Watoto wake watakuwa wenye uwezo katika nchi, kizazi cha watu waadilifu kitabarikiwa.
3
Nyumbani mwake kuna mali na utajiri, haki yake hudumu milele.
4
Hata gizani nuru humzukia mtu mwadilifu, yule mwenye rehema, huruma na haki.
5
Mema yatamjia mtu yule aliye mkarimu na mwenye kukopesha bila riba, anayefanya mambo yake kwa haki.
6
Hakika hatatikisika kamwe, mtu mwenye haki atakumbukwa milele.
7
Hataogopa habari mbaya, moyo wake ni thabiti, ukimtegemea Bwana.
8
Moyo wake ni salama, hatakuwa na hofu, mwishoni ataona ushindi dhidi ya adui zake.
9
Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini; haki yake hudumu milele; pembe yake itatukuzwa kwa heshima.
10
Mtu mwovu ataona na kuchukizwa, atasaga meno yake na kutoweka, kutamani kwa mtu mwovu kutaishia patupu.
Global Bible Tools - Collaborative Bible translation platform